Saturday, May 12, 2012

Demokrasia ya Tanzania yapigiwa mfano duniani

IMEBAINISHWA kuwa demokrasia iliyopo Tanzania ni moja wapo ya chachu inayowafanya watu wengi zikiwemo nchi zilizoendelea duniani kutamani kuwa nayo, lakini inashindikana kutokana na mifumo yao ya kiutawala.

Mbali na hayo Watanzania wamehimizwa kuendelea kuilinda, kuheshimu na kuitumia vyema demokrasia hiyo katika kujadili ikiwemo kuibua mambo ambayo hayana uchochezi ili kuharakisha maendeleo yao.

Changamoto hiyo ilitolewa juzi na Waziri Mkuu mstaafu wa Rwanda Bw. Faustine Twagiramungu ambaye kwa sasa anaishi mjini Brussels nchini Ubeligiji wakati akichangia mada kwenye kipindi cha Straight Talk Afrika ambacho huwa kinarushwa na Sauti ya Amerika (VOA) kutoka mjini Washington DC nchini Marekani.

Hata hivyo sababu kuu iliyomsukuma Waziri huyo mstaafu kutamka hivyo ni kutokana na mada ambayo iliwasilishwa katika kipindi hicho ambayo iliangazia tija ambayo inaweza kupatikana kwa Bara la Afrika baada ya Wafaransa kufanya uamuzi wa kidemokrasia na kumuingiza madarakani Bw. Francois Hollande.

"Huwezi kumpima mtu kwa matendo yake ila uamuzi na siasa safi hususan demokrasia zenye mantiki kwa Afrika ndizo kimbilio na ufunguo wa maendeleo kwa Afrika;

"Nikiwa huku nilipo (Ubeligiji) nchi ambazo ninaweza kujivunia kuwa na demokrasia ya kweli si kwetu Rwanda... ni Tanzania na ninaamini iwapo wataitukuza (Watanzania) demokrasia hiyo ni fundisho pekee na mfano wa kuigwa katika Bara la Afrika na hata nje ya bara letu," alisema Bw. Twagiramungu.

Hata hivyo baadhi ya wachangiaji wa mada hiyo kutoka sehemu mbalimbali duniani walisema kuwa, nchi za Afrika ikiwemo Tanzania haziwezi kutegemea wahisani kuziendesha ila umefika wakati sasa rasilimali zinazowazunguka kutumika vyema kwa manufaa ya Waafrika.

"Kuchaguliwa kwa Rais mpya nchini Ufarasa kwetu (Afrika) si tija, haijalishi sera zake zinajikita katika Ujamaa au la!...tutakachofanya ni kuendelea kudumisha umoja na ushirikiano, lakini masuala ya uwajibikaji kwa manufaa ya nchi zetu yanatuhusu wenyewe," alisema mmoja wa wachangiaji wa mada hiyo kutoka nchini Nigeria.

Hata hivyo tafiti zinaonesha kuwa mbali na changamoto za hapa na pale demokrasia iliyopo Tanzania imekuwa mfano wa kuigwa kutokana na Watanzania wenyewe kuwa na maamuzi yao pekee bila kulazimishwa na watu ya kuwachagua ikiwemo kuwakataa viongozi ambao wanaona hawawajibiki ipasavyo.